Monday, April 3, 2017

Uzalendo na utaifa vinajengwa na viongozi wakubwa sio wananchi kama tunavyofikiria
Neno uzalendo linahubiriwa sana  kwa vijana wa Tanzania. Viongozi wakubwa wanahubiri hivyo. Lakini ukweli ni kwamba uzalendo unaanza kujengwa na viongozi wa ngazi za juu Kama marais, mawaziri, wabunge, kwakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya pamoja na viongozi wengine ambao ni wafanyakazi wa serikali wa kuajiriwa.


Ni vigumu kijana kuipenda nchi yake kama kijana huyu anashindwa kupata ajira, kijana huyu akienda sokoni vitu bei juu, Kijana huyu hata sehemu ya kulala kwake ni shida. Tuchukulie mfano Baba wa familia akihubiri uzalendo kwa watoto wake wakati watoto hawafurahii maisha jinsi yanavyoendeshwa kwenye familia hiyo.  Vijana hawa hata wakihubiriwa uzalendo mara elfu moja hawawezi kuwa na uzalendo na familia yao.

Uzalendo ni "involuntary action" Uzalendo unakuja automatically bila kulazimishwa au kusisitizwa na viongozi. Matendo vya viongozi kwa wananchi wao ndiyo yatakayowafanya wanachi kuwa na uzalendo au wasiwe na uzalendo. Kama viongozi watakuwa mafisadi, hawatendi haki sawa kwa wote pamoja na maovu mengine yanayoonekana na yasiyoonekana basi jamii wanayoiongoza lazima nayo ikose uzalendo.

Uzalendo ni kama upendo ukimpenda mtu naye atakupenda. Ukimwonesha uzalendo mwanachi basi naye mwananchi ataonesha uzalendo kwako hatimaye kitendo hiki kitajenga uzalendo kwa Taifa zima. Kama wananchi wanalalamikia uongozi uliopo madarakani kwa masuala mbalimbali kama vile kutosaidiwa kujikwamua kwenye wimbi la umaskini ni dhahirii kuwa wananchi nao hawatakuwa na uzalendo na serikali yao pamoja na taifa kwa ujumla.

Hayati mwalimu Julius kambarage nyerere alionesha uzalendo mkubwa kwa Taifa la Tanzania pamoja na Raia wa Tanzania ndio maana vijana wa muda huo walikuwa tayari hata kuifia nchi yao. Lakini leo hii sina uhakika kama vijana asilimia ngapi wanaweza kuitetea Tanzania ipasavyo kwa lugha nyingine kuwa na uzalendo. Kama kijana yupo tayari aende china akanunue bidhaa feki zenye madhara kwa Taifa la Tanzania ilimradi ajikwamue kiiuchumi baada ya kushindwa kufanikiwa kwa njia halali nchini mwake hii ni dalili ya kupoteza uzalendo. Viongozi tuna jukumu la kuwasaidia vijana hawa waweze kufanikiwa kwa kutumia fulsa halali zilizopo nchini mwao.

Tujitathmini je Sekta ya biashara ni rafiki kwa mfanyabiashara je sekta ya kilimo nayo ipo sawa? ni kweli kijana akisomea kilimo akaenda benki kukopa mtaji na kuwekeza kwenye kilimo atafanikiwa na kutengeneza ajira kwa vijana wengine? Haya ni baadhi tu ya maswali ya kujiuliza. Hapa ndipo Kiongozi unatakiwa kuumiza kichwa kutengeneza mazingira mazuri kwa wananchi wako toka moyoni sio tu kwa kuonekana kwenye Taarifa za habari.

Mwajiri umeajiri wafanyakazi kwenye taasisi yako anza wewe kuonesha uzalendo wajali wafanyakazi wako ili nao wajali taasisi yako. Ukibaki kutumia motivation za adhabu ukidhani ndo unawarekebisha watumishi wako ili upate matokeo mazuri inaweza kuwa kinyume chake. Uzalendo wa taasisi yako unaanza na wewe mkurugenzi wa taasisi husika, sio kwa kuwahubiria wafanyakazi wako kuwa wapende taasisi yako wapendende kazi wanazofanya kwenye taasisi yako wakati wewe huwapendi.

Baba wa familia ukitumia ubabe kuongoza familia yako basi utapata heshima za woga za ndiyo mkuu wakati upande wa pili wa pazia wanafamilia hawatakuwa na mapenzi na familia hiyo kwaku hawajisikii toka moyoni kuwa na uzalendo na familia hiyo.

Tujifunze uzalendo ni nini? Vitu gani vinasababisha jamii kuwa na uzalendo na Taifa lake?